Nilianza
kumfahamu msanii Khaleed Mohammed au Top in Dar (TID) alipotoa wimbo
pendwa wa Zeze miaka ile ya 2000s akiwa na Jay Moe..
Jina lake likakua na kukubalika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania huku
akijivunia sauti yake na kujiita 'Golden Voice' yaani Sauti ya Dhahabu,
jina ambalo alilipa album yake ya kwanza iliyojaa nyimbo zilizobamba
tupu kwa wakati huo..
Kuna kituo maarufu cha redio, kiliwahi kutumia sauti yake kufanyia
'jingle' matata sana kwa miaka mingi kabla TCRA haijabadili 'masafa' kwa
vituo vya redio zote nchini. Ile Jingle ni shida (92.9, Magic Fm, Dar
es salaam)..
Historia tamu ya SAUTI YA DHAHABU ninayo, ila kwa leo acha niishie hapo.
Kucheza? Nani hakumbuki 'shekisheki' za TID zilivyovuruga vijana mitaani
kwetu? Kuna aliyesahau kwamba TID ndiye msanii pekee aliyebuni michezo
mingi ya kuvunja (breakdance) hapa Bongo, kiasi cha kupachikwa jina la
'Wacko Jacko', likimaanisha 'Michael Jackson', jina la mfalme wa muziki
wa Pop na 'michezo ya kuvunja' duniani (apumzike kwa amani).
Jina la TID liliuza magazeti, lilivuta mapromota (mameneja waliitwa
mapromota wakati huo), lilileta hamasa ya vipindi vya muziki kwenye
televisheni zetu nchini.. Alitamba kila siku.. Alikuwa NEMBO ya muziki
wa kizazi kipya..
TID alijua kuimba na kucheza. Andaa show, usimuite TID, imekula kwako!
Inakadiriwa kuwa ndiye mwanamuziki wa kwanza kwenda kufanya ziara ya
kimuziki Uingereza. Yes, wa kwanza kutoka Bongoflevani. Huko akafyatua
na video ya wimbo wake wa 'Pekee'. Wapo waliokoma kwa hili!
Sijasahau, umaarufu wa TID ndio uliibeba filamu bora ya maisha na muziki
kuwahi kutokea hapa nchini, Girlfriend, akiwa kama mhusika mkuu
akishirikiana na dada Monalisa wa Natasha. Hata leo hii, tunakubaliana
kwamba hapakuwahi kutokea filamu ya Kiswahili iliyotazamwa na kukubalika
nchini zaidi ya hiyo. Kila mtu alimwangalia zaidi TID humo. Mungu
ampumzishe kwa amani mtayarishaji George Tyson.
Hayo yamepita.
Kuna fani TID aliyosomea. Fani ya Utangazaji. Sio kusomea tu, huko ndiko
alikotokea kabla ya kuingia kwenye muziki. Wengi hawakulijua hili la
utangazaji mpk pale jina lake lilipokuwa kubwa kupitia muzikia.. Mimi
nikiwa mmojawapo. Kama kuna ambaye halijui hilo, habari imfikie rasmi
leo.
Ngoja nikueleze, TID alikuwa anasifika kwa umahiri wa kutangaza redioni.
Hakuwa maarufu kwa sana, lakini alikuwa hodari na machachari sana akiwa
nyuma ya maiki. Sifa yake kubwa ilikuwa ni sauti ya bashasha na umahiri
wa kutumia lugha ya kiingereza 'kimjini mjini'. Acha bwana! Ulikuwa
ukimsikiliza TID siku za weekend usiku, hata kama ulikuwa na mpango wa
kwenda club utaghairi. Taji Liundi heshima kwako kwa kukivumbua hiki
kipaji..
Sina data nyingi kuhusu 'utangazaji' wa TID, lakini naamini ni kitu
anachoweza kufanya zaidi na kukubalika hasa katika kipindi hiki ambacho
muziki una 'vurugu' na fitina za kutosha.
Hapa namuwazia Mtangazaji TID mwenye makeke lakini yasiyo na utani
utani. Namjengea picha akiwa ni mtangazaji anayeheshimu wasikilizaji
wake na mwenye nidhamu ya kazi.
Nani asingependa kumsikiliza TID nyakati za jioni? Rudi kazini TIDI.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon