SERIKALI ‘YAPIGA STOP’ UVAAJI WA MAJOHO SHULENI, VYUO DIPLOMA


WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amepiga marufuku matumizi ya joho kwenye sherehe za mahafali ya ngazi za chini za elimu na kutaka litumike kuanzia ngazi ya shahada ili kulipa heshima vazi hilo.
Waziri Ndalichako aliyasema hayo juzi jijini Mbeya alipokuwa anawatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa njia ya masafa, iliyotolewa na Wakala wa Usimamizi na Uongozi wa Elimu (Adem).
Alisema katika kipindi hiki ambacho serikali inafanya jitihada za kuboresha sekta ya elimu ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni lazima kutofautisha ngazi za elimu ili mwanafunzi wa ngazi ya chini atamani kufika ngazi ya juu.
Alisema kwa sasa vazi hilo linaonekana kuwa ni la kawaida kwa kuvaliwa na wanafunzi mpaka wa darasa la awali hali ambayo alisema haitakiwi kuendelea na badala yake livaliwe na wanafunzi wa kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea.
“Kila ngazi ya elimu ina heshima yake, hivyo hiyo heshima inatakiwa iendelee kubaki hivyo ili mwanafunzi wa ngazi ya chini atamani kufikia ngazi inayofuata na kwa hali hiyo, wanafunzi watajibidisha kwa kiasi kikubwa ili kuzifikia ngazi hizo.
Kwa sasa unakuta wanafunzi wa ngazi ya awali wanavaa joho, shule za msingi hivyo hivyo na mtu wa shahada anavaa hivyo hivyo, sasa nataka hilo vazi liwe la wanafunzi wa kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza,” alisema.
Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo walikubaliana na maelezo ya Waziri Ndalichako kwa madai kuwa vazi hilo kwa sasa linakosa heshima yake na kwamba liendelee kubaki kwa ajili ya watu wa shahada na kuendelea.
Kwenye sherehe hizo, wahitimu 860 wa mafunzo hayo walitunukiwa vyeti na Waziri Ndalichako na aliwataka kutumia taaluma waliyoipata katika mafunzo hayo ili kuinua elimu nchini.
Previous
Next Post »