Aliyekuwa
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, SP Christopher Bageni
amewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya
kunyongwa hadi kufa.
SP Bageni alihukumiwa adhabu hiyo baada
ya mahakama hiyo kujiridhisha kwamba aliwaua kwa kukusudia
wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva
teksi mkazi wa Manzese, Dar es Salaam, katika Msitu wa Pande.
Bageni kupitia Wakili wake, Gaudioz
Ishengoma, aliwasilisha maombi hayo mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na
hati ya kiapo iliyoapwa na wakili huyo.
Muwasilisha maombi anaomba mahakama hiyo
kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa
Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza. Akitoa sababu kuomba marejeo, anadai
alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi ulioko
kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa
mashtaka.
Alidai katika kuchanganua ushahidi ambao
uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika na ushahidi wa
msingi (Exam in Chief) wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu
tu ushahidi wa utetezi hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa. Katika hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili
Ishengoma, Bageni anadai yeye na wengine wanane ambao hawako katika
maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa
ya mauaji ya watu wanne katika Kesi ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.
Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na
katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati, amnayo wote waliachiwa
huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo
hivyo alikata rufaa namba 358 ya mwaka 2013. Kabla ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP
aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne
ambao waliachiwa huru pia Septemba 16, mwaka huu.
Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu wa
Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi
Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili baada ya mahakama kuona hakuna
ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia hatiani.
Katika kesi ya msingi, Bageni alidaiwa
kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na
ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa
dereva wa teksi wa Manzese mnamo Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu
wa Pande, Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon